Ezekiel (39/48)  

1. Na wewe, mwanadamu, tabiri juu ya Gogu, useme, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Gogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali;
2. nami nitakugeuza na kukuongoza, nami nitakupandisha toka pande za mwisho za kaskazini; nami nitakuleta juu ya milima ya Israeli;
3. nami nitaupiga upinde wako, utoke katika mkono wako wa kushoto, na mishale yako nitaiangusha, itoke katika mkono wako wa kulia.
4. Utaanguka juu ya milima ya Israeli, wewe, na vikosi vyako vyote, na watu wa kabila nyingi walio pamoja nawe; nami nitakutoa na kuwapa ndege wa kila namna walao nyama, na wanyama wa nchi, uliwe na wao.
5. Utaanguka katika uwanda; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
6. Nami nitapeleka moto juu ya Magogu; na juu ya watu wote wakaao salama katika visiwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
7. Na jina langu takatifu nitalifanya kuwa limejulika kati ya watu wangu Israeli; wala sitaliacha jina langu takatifu kutiwa unajisi tena; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, na Aliye Mtakatifu katika Israeli.
8. Tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU; hii ndiyo siku ile niliyoinena.
9. Hao wakaao katika miji ya Israeli watatoka, nao watafanya mioto kwa silaha za vita na kuziteketeza, ngao, na vigao, na pinde, na mishale, na mafumo, na mikuki, nao watazitumia kama kuni kwa muda wa miaka saba;
10. hata hawataokota kuni mashambani, wala hawatakata kuni msituni; maana watafanya mioto kwa silaha zile; nao watawateka nyara watu waliowateka wao, na kunyang'anya vitu vya watu walionyang'anya vitu vyao, asema Bwana MUNGU.
11. Tena, itakuwa katika siku hiyo, nitampa Gogu pa kuzikia katika Israeli, bonde la wapitao, upande wa mashariki wa bahari; nalo litawazuia wapitao; na huko watamzika Gogu na watu wake jamii yote; nao wataliita, Bonde la Hamon-Gogu.
12. Na kwa muda wa miezi saba nyumba ya Israeli watakuwa wakiwazika, wapate kuisafisha nchi.
13. Naam, watu wote wa nchi hiyo watawazika; itakuwa ni sifa kwao katika siku ile nitakapotukuzwa, asema Bwana MUNGU.
14. Nao watawachagua watu wa kufanya kazi ya daima, watakaopita kati ya nchi, ili kuwazika waliosalia juu ya uso wa nchi, ili kuisafisha; miezi saba itakapokwisha kupita watatafuta.
15. Na hao wapitao kati ya nchi watatafuta; na mtu ye yote aonapo mfupa wa mtu, ndipo atakapoweka alama karibu nao, hata wazishi watakapouzika katika bonde la Hamon-Gogu.
16. Tena, Hamona litakuwa jina la mji. Hivyo ndivyo watakavyosafisha nchi.
17. Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Sema na ndege wa kila namna, na kila mnyama wa kondeni, Jikusanyeni, mje; jikusanyeni pande zote mwijilie sadaka yangu niifanyayo kwa ajili yenu, naam, sadaka kubwa juu ya milima ya Israeli, mpate kula nyama na kunywa damu.
18. Mtakula nyama yao walio hodari, na kunywa damu ya wakuu wa dunia, ya kondoo waume na ya wana-kondoo, na ya mbuzi, na ya ng'ombe, wote na wanono wa Bashani.
19. Nanyi mtakula mafuta na kushiba, mtakunywa damu na kulewa, na sadaka yangu niliyoifanya kwa ajili yenu.
20. Nanyi mtashibishwa mezani pangu kwa farasi, na magari ya vita, na mashujaa, na watu wote wa vita, asema Bwana MUNGU.
21. Nami nitauweka utukufu wangu kati ya mataifa, na mataifa wote wataiona hukumu yangu niliyoitekeleza, na mkono wangu niliouweka juu yao.
22. Basi, nyumba ya Israeli watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, tangu siku hiyo na baadaye.
23. Nao mataifa watajua ya kuwa nyumba ya Israeli walihamishwa, na kwenda kifungoni, kwa sababu ya uovu wao; kwa sababu waliniasi, nami nikawaficha uso wangu; basi nikawatia katika mikono ya adui zao, nao wakaanguka kwa upanga, wote pia.
24. Kwa kadiri ya uchafu wao, kwa kadiri ya makosa yao, ndivyo nilivyowatenda, nami nikawaficha uso wangu.
25. Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Sasa nitawarejeza watu wa Yakobo waliohamishwa, nitawahurumia nyumba yote ya Israeli; nami nitalionea wivu jina langu takatifu.
26. Nao watachukua aibu yao, na makosa yao yote waliyoniasi, watakapokaa salama katika nchi yao wenyewe, wala hapana mtu atakayewatia hofu;
27. nitakapokuwa nimewaleta tena kutoka kabila za watu, na kuwakusanya kwa kuwatoa katika nchi za adui zao, na kutakaswa kati yao mbele ya macho ya mataifa mengi.
28. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, kwa kuwa naliwahamisha, waende utumwani kati ya mataifa, na mimi nikawakusanya, na kuwaingiza katika nchi yao wenyewe; wala sitawaacha tena huko kamwe, hata mmojawapo;
29. wala sitawaficha uso wangu tena; kwa maana nimemwaga roho yangu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.

  Ezekiel (39/48)