Ezekiel (37/48)  

1. Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa;
2. akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana.
3. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.
4. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana.
5. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
6. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
7. Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
8. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake.
9. Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi.
10. Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
11. Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.
12. Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli.
13. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu.
14. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema Bwana.
15. Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
16. Na wewe mwanadamu, twaa kijiti kimoja; ukaandike juu yake, Kwa Yuda, na kwa wana wa Israeli wenzake; kisha, twaa kijiti cha pili; ukaandike juu yake, Kwa Yusufu, kijiti cha Efraimu, na kwa nyumba yote ya Israeli wenzake;
17. ukaviunge pamoja kwa ajili yako hiki na hiki viwe kijiti kimoja, viwe kimoja katika mkono wako.
18. Na wana wa watu wangu watakapokuambia, wakisema, Je! Hutatuonyesha maana ya mambo hayo utendayo?
19. Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitakitwaa kijiti cha Yusufu, kilicho mkononi mwa Efraimu, na kabila za Israeli wenzake, nami nitawaweka pamoja nacho, yaani, pamoja na kijiti cha Yuda, na kuvifanya kuwa kijiti kimoja; navyo vitakuwa kimoja mkononi mwangu.
20. Navyo vijiti, ambavyo uliandika juu yake, vitakuwa mkononi mwako mbele ya macho yao.
21. Ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe;
22. nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena, hata milele.
23. Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makosa yao mojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
24. Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda.
25. Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mkuu wao milele.
26. Tena nitafanya agano la amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; nami nitawaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele.
27. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
28. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.

  Ezekiel (37/48)