← Ezekiel (35/48) → |
1. | Tena neno la Bwana likanijia, kusema, |
2. | Mwanadamu, kaza uso wako juu ya mlima Seiri, ukatabiri juu yake, |
3. | uuambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima Seiri, nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, nami nitakufanya kuwa ukiwa na ajabu. |
4. | Miji yako nitaiharibu, nawe utakuwa ukiwa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
5. | Kwa kuwa umekuwa na uadui usiokoma, nawe umewatoa wana wa Israeli wapigwe kwa nguvu za upanga, wakati wa msiba wao, wakati wa mwisho wa uovu. |
6. | Basi, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, nitakuweka tayari kwa damu, na damu itakufuatia; ikiwa hukuchukia damu, basi damu itakufuatia. |
7. | Hivyo ndivyo nitakavyoufanya mlima Seiri kuwa ajabu na ukiwa; nami nitakatilia mbali nao mtu apitaye, na mtu arejeaye. |
8. | Nami nitaijaza milima yake watu wake waliouawa; katika milima yako, na katika mabonde yako, na katika mifereji yako ya maji yote, wataanguka wao watakaouawa kwa upanga. |
9. | Nitakufanya kuwa ukiwa wa daima, na miji yako haitakaliwa na watu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
10. | Kwa sababu umesema, Mataifa haya mawili na nchi hizi mbili zitakuwa zangu, nasi tutazimiliki, ijapokuwa Bwana alikuwako huko. |
11. | Basi, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, nitatenda kwa kadiri ya hasira yako, na kwa kadiri ya wivu wako, ulioudhihirisha kwa kuwachukia; nami nitajidhihirisha kwao, nitakapokuhukumu wewe. |
12. | Nawe utajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeyasikia matukano yako yote, uliyoyanena juu ya milima ya Israeli, ukisema, Wamefanyika ukiwa, wametiwa katika mikono yetu tuwale. |
13. | Nanyi mmejitukuza juu yangu kwa vinywa vyenu, na kuyaongeza maneno juu yangu; nimesikia mimi. |
14. | Bwana MUNGU asema hivi; Dunia yote itakapofurahi, nitakufanya kuwa ukiwa. |
15. | Kama vile ulivyofurahi juu ya urithi wa nyumba ya Israeli, kwa sababu ilikuwa ukiwa, ndivyo nitakavyokutenda wewe; utakuwa ukiwa, Ee mlima Seiri, na Edomu yote, naam, yote pia; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
← Ezekiel (35/48) → |