Ezekiel (34/48)  

1. Neno la Bwana likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?
3. Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.
4. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala.
5. Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama-mwitu, wakatawanyika.
6. Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta.
7. Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;
8. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu;
9. kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;
10. Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.
11. Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia.
12. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.
13. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.
14. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.
15. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.
16. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.
17. Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo waume na mbuzi waume pia.
18. Je! Mwaona ya kuwa ni neno dogo ninyi kulishwa malisho mema, hata mkawa hamna budi hukanyaga kwa miguu yenu yaliyosalia? Na kuwa mmekunywa maji yaliyo safi, nanyi hamna budi kuyatibua kwa miguu yaliyobaki?
19. Na kwa habari za kondoo zangu, wao wanakula hayo mliyoyakanyaga kwa miguu yenu, nao wanakunywa maji mliyoyatibua kwa miguu yenu.
20. Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU awaambia hivi; Tazama, mimi, naam, mimi, nitahukumu kati ya wanyama walionona na wanyama waliokonda.
21. Kwa kuwa mmesukuma kwa ubavu, na kwa mabega, na kuwapiga wenye maradhi kwa pembe zenu, hata mkawatawanyia mbali;
22. basi mimi nitaliokoa kundi langu, wala hawatakuwa mateka tena; nami nitahukumu kati ya mnyama na mnyama.
23. Nami nitaweka mchungaji mmoja juu yao, naye atawalisha, naam, mtumishi wangu, Daudi; yeye atawalisha, naye atakuwa mchungaji wao.
24. Na mimi, Bwana, nitakuwa Mungu wao, na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mkuu kati yao; mimi, Bwana, nimesema haya.
25. Nami nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.
26. Nami nitawafanya wao, na mahali palipo pande zote za mlima wangu, kuwa baraka, nami nitaleta manyunyu kwa wakati wake; yatakuwako manyunyu ya baraka.
27. Na mti wa kondeni utazaa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, nao watakuwa salama katika nchi yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapovunja vifungo vya kongwa lao, na kuwaokoa katika mikono ya watu wale waliowatumikisha.
28. Hawatakuwa mateka ya makafiri tena, wala mnyama wa nchi hatawala; bali watakaa salama salimini, wala hapana mtu atakayewatia hofu.
29. Nami nitawainulia miche iwe sifa njema, wala hawataangamizwa kwa njaa katika nchi yao tena, wala hawatachukua tena aibu ya makafiri.
30. Nao watajua ya kuwa mimi, Bwana, Mungu wao, ni pamoja nao, na ya kuwa wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana MUNGU.
31. Na ninyi, kondoo zangu, kondoo za malisho yangu, ni wanadamu, na mimi ni Mungu wenu, asema Bwana MUNGU.

  Ezekiel (34/48)