Ezekiel (3/48)  

1. Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.
2. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.
3. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.
4. Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.
5. Maana wewe hukutumwa kwa watu wa maneno mageni, ama wa lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli;
6. si kwa watu wa kabila nyingi wenye maneno mageni, na lugha ngumu, ambao huwezi kufahamu maneno yao. Bila shaka, kama ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.
7. Bali nyumba ya Israeli hawatakusikiliza wewe; kwa kuwa hawanisikilizi mimi; maana nyumba yote ya Israeli wana vipaji vigumu, na mioyo yenye ukaidi.
8. Tazama, nimeufanya uso wako kuwa mgumu juu ya nyuso zao, na kipaji cha uso chako kuwa kigumu juu ya vipaji vya nyuso vyao.
9. Kama almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji chako; usiwaogope, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.
10. Tena akaniambia, Mwanadamu, maneno yangu yote nitakayokuambia, yapokee moyoni mwako, na kuyasikia kwa masikio yako.
11. Haya! Enenda uwafikilie watu hao waliohamishwa, kwa wana wa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, Bwana MUNGU asema hivi; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia.
12. Ndipo roho ikaniinua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama mshindo wa radi kuu, ikisema, Na uhimidiwe utukufu wa Bwana tokea mahali pake.
13. Nikasikia mshindo wa mabawa ya vile viumbe hai, walipogusana, na mshindo wa yale magurudumu kando yao, mshindo wa radi kuu.
14. Basi roho ikaniinua, ikanichukua mahali pengine; nami nikaenda kwa uchungu, na hasira kali rohoni mwangu, na mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu kwa nguvu.
15. Ndipo nikawafikia watu waliohamishwa, huko Tel-abibu, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari, nikafika huko walikokuwa wakikaa; nikaketi huko miongoni mwao muda wa siku saba, katika hali ya ushangao mwingi.
16. Hata ikawa, mwisho wa siku saba, neno la Bwana likanijia, kusema,
17. Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.
18. Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
19. Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.
20. Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
21. Bali ukimwonya mwenye haki, kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikiwa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa; nawe umejiokoa roho yako.
22. Na mkono wa Bwana ulikuwako juu yangu huko; akaniambia, Ondoka, enenda uwandani; nami nitasema nawe huko.
23. Basi, nikaondoka, nikaenda uwandani, na tazama, utukufu wa Bwana ulisimama huko, kama utukufu ule niliouona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24. Ndipo roho ile ikaniingia, ikanisimamisha kwa miguu yangu; akasema nami, akaniambia, Enenda ukajifungie nyumbani mwako.
25. Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu, nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao;
26. nami nitaufanya ulimi wako ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao; kwa kuwa wao ni nyumba yenye kuasi.
27. Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua kinywa chako, nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Yeye asikiaye na asikie; naye akataaye na akatae; maana wao ni nyumba yenye kuasi.

  Ezekiel (3/48)