← Ezekiel (29/48) → |
1. | Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema, |
2. | Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote; |
3. | nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu. |
4. | Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako. |
5. | Nami nitakuacha hali umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka juu ya uso wa uwanda; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani. |
6. | Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli. |
7. | Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote. |
8. | Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama. |
9. | Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya. |
10. | Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi. |
11. | Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arobaini. |
12. | Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali. |
13. | Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao; |
14. | nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni. |
15. | Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hautajiinua tena juu ya mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya mataifa. |
16. | Wala hautakuwa tena tumaini la nyumba ya Israeli, kufanya maovu yakumbukwe, watakapogeuka kuangalia nyuma yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU. |
17. | Ikawa katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema, |
18. | Mwanadamu, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alilihudumisha jeshi lake huduma kuu juu ya Tiro; kila kichwa kilitiwa upaa, na kila bega liliambuliwa ngozi, lakini alikuwa hana mshahara uliotoka Tiro, wala yeye wala jeshi lake, kwa huduma ile aliyohudumu juu yake. |
19. | Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitampa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, hiyo nchi ya Misri; naye atawachukua watu wake jamii yote pia, na kutwaa mateka yake, na kutwaa mawindo yake, nayo yatakuwa ndio mshahara wa jeshi lake. |
20. | Nimempa nchi ya Misri kuwa malipo ya huduma aliyohudumu, kwa sababu walifanya kazi kwa ajili yangu; asema Bwana MUNGU. |
21. | Siku ile nitawachipushia nyumba ya Israeli pembe, nami nitakujalia kufumbua kinywa kati yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
← Ezekiel (29/48) → |