Ezekiel (27/48)  

1. Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2. Na wewe, mwanadamu, mfanyie Tiro maombolezo;
3. umwambie Tiro, Ewe ukaaye penye maingilio ya bahari, uliye mchuuzi wa watu wa kabila nyingi, mpaka visiwa vingi, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe, Tiro, umesema, Mimi ni ukamilifu wa uzuri.
4. Mipaka yako i kati ya moyo wa bahari; wajenzi wako wameukamilisha uzuri wako.
5. Mbao zako zote wamezifanya kwa misunobari itokayo Seniri; wametwaa mierezi ya Lebanoni ili kukufanyia mlingoti;
6. kwa mialoni ya Bashani wamefanya makasia yako; na sitaha zako wamezifanya kwa pembe iliyotiwa kazi ya njumu katika mti wa mihugu itokayo Kitimu.
7. Tanga lako lilikuwa la kitani safi itokayo Misri, iliyotiwa taraza, ili iwe bendera kwako; na chandalua chako kilikuwa cha rangi ya samawi na urujuani toka visiwa vya Elisha.
8. Wakaao Sidoni na Arvadi ndio waliovuta makasia yako; wana wako wenye akili, Ee Tiro, walikuwa ndani yako, ndio waliokuwa rubani zako.
9. Wazee wa Gebali na wenye akili wake walikuwa ndani yako, wenye kutia kalafati; merikebu zote za bahari na mabaharia wao walikuwa ndani yako, ili kubadiliana biashara yako.
10. Watu wa Uajemi na Ludi na Putu walikuwa katika jeshi lako, watu wako wa vita; walitungika ngao na chapeo ndani yako; wakadhihirisha uzuri wako.
11. Watu wa Arvadi, pamoja na jeshi lako, walikuwa juu ya kuta zako pande zote, na Wagamadi walikuwa ndani ya minara yako; walitungika ngao zao juu ya kuta zako pande zote; wakaukamilisha uzuri wako.
12. Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
13. Uyunani na Tubali na Mesheki ndio waliokuwa wachuuzi wako; walitoa wanadamu, na vyombo vya shaba, kwa biashara yako.
14. Watu wa nyumba ya Togarma walifanya biashara, kwa farasi, naam, farasi za vita, na nyumbu, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
15. Wadedani walikuwa wachuuzi wako, visiwa vingi vilikuwa soko la mkono wako; walikuletea pembe, na mpingo, ili kuvibadili.
16. Shamu alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa kazi za mkono wako walifanya biashara kwa zumaridi, na urujuani, na kazi ya taraza, na kitani safi, na marijani, na akiki, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
17. Yuda, na nchi ya Israeli, walikuwa wachuuzi wako; walitoa badala ya bidhaa yako ngano ya Minithi, na mtama, na asali, na mafuta, na zeri.
18. Dameski alikuwa mfanya biashara kwako, kwa habari ya wingi wa kazi za mkono wako, kwa ajili ya wingi wa aina zote za utajiri; akaleta divai ya Helboni, na sufu nyeupe.
19. Wedani, na Yavani, walifanya biashara toka Uzali kwa vitu vyako; chuma kilichofuliwa, na mdalasini, na mchai, vilikuwa katika bidhaa yako.
20. Dedani alikuwa mchuuzi wako, kwa nguo za thamani za kutandikia farasi.
21. Arabuni, na wakuu wote wa Kedari, ndio waliokuwa wafanya biashara wa mkono wako; kwa wana-kondoo, na kondoo waume, na mbuzi; kwa hao walifanya biashara nawe.
22. Wachuuzi wa Sheba, na Raama, ndio waliokuwa wachuuzi wako; badala ya vitu vyako walitoa manukato yaliyo mazuri, na kila aina ya vito vya thamani, na dhahabu.
23. Harani, na Kane, na Adini, wachuuzi wa Sheba, na Ashuru, na Kilmadi, walikuwa wachuuzi wako.
24. Hao ndio waliokuwa wachuuzi wako, kwa vitu vya tunu, kwa vitumba vya nguo za samawi na kazi ya taraza, na masanduku ya mavazi ya thamani, yaliyofungwa kwa kamba, na kufanyizwa kwa mti wa mierezi, katika bidhaa yako.
25. Merikebu za Tarshishi zilikuwa misafara yako, kwa bidhaa yako; nawe ulijazwa sana, ukawa mtukufu sana, katika moyo wa bahari.
26. Wavuta makasia wako walikuleta katika maji makuu; upepo wa mashariki umekuvunja moyoni mwa bahari.
27. Mali zako, na bidhaa yako, na utajiri wako, wana-maji wako, na rubani zako, na wenye kutia kalafati wako, na wafanya biashara wako, na watu wako wa vita wote, walio ndani yako, pamoja na jeshi lako lote lililo ndani yako, wataanguka katika moyo wa bahari katika siku ya kuangamia kwako.
28. Kwa sauti ya vilio vya rubani zako viunga vyako vitatetema.
29. Na wote wavutao kasia, wana-maji, na rubani zote wa baharini, watashuka katika merikebu zao, na kusimama katika nchi kavu;
30. nao watasikizisha watu sauti zao juu yako, nao watalia kwa uchungu, na kutupa mavumbi juu ya vichwa vyao, na kugaagaa katika majivu;
31. nao watajifanya kuwa na upaa kwa ajili yako, na kujifunga nguo za magunia viunoni, nao watakulilia kwa uchungu wa roho, kwa maombolezo ya uchungu.
32. Na katika kulia kwao watakufanyia maombolezo, na kukuombolezea, wakisema, Ni nani aliye kama Tiro, kama yeye aliyenyamazishwa kati ya bahari?
33. Bidhaa zako zilipotoka katika bahari, uliwajaza watu wa kabila nyingi; uliwatajirisha wafalme wa dunia, kwa wingi wa mali zako, na kwa utajiri wako.
34. Wakati ulipovunjwa na bahari, katika vilindi vya maji, bidhaa zako na jeshi lako lote walianguka kati yako.
35. Wote wakaao katika visiwa vile watakustaajabia, na wafalme wao wameogopa sana, wamefadhaika nyuso zao.
36. Wafanya biashara kati ya kabila za watu wakuzomea; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena milele.

  Ezekiel (27/48)