← Ezekiel (26/48) → |
1. | Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema, |
2. | Mwanadamu, Kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemu, Aha! Yeye amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika; |
3. | basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake. |
4. | Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu. |
5. | Naye atakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi kati ya bahari; maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU; naye atakuwa mateka ya mataifa. |
6. | Na binti zake walio katika mashamba watauawa kwa upanga; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
7. | Maana Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitamleta Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mfalme wa wafalme, juu ya Tiro toka kaskazini, pamoja na farasi, na magari ya vita, na wapanda farasi, na jeshi, na watu wengi. |
8. | Atawaua binti zako kwa upanga katika mashamba; naye atafanya ngome juu yako, na kufanya maboma juu yako, na kuiinua ngao juu yako. |
9. | Naye ataweka vyombo vyake vya kubomolea mbele za kuta zako, na kwa mashoka yake ataiangusha chini minara yako. |
10. | Kwa sababu wingi wa farasi zake, mavumbi yao yatakufunika; kuta zako zitatetemeka kwa sababu ya mshindo wa wapanda farasi, na wa magurudumu, na wa magari ya vita, atakapoingia katika malango yako, kama watu waingiavyo katika mji uliobomolewa mahali. |
11. | Kwa kwato za farasi zake atazikanyaga njia zako zote; atawaua watu wako kwa upanga, na minara ya nguvu zako itashuka hata nchi. |
12. | Nao wataufanya utajiri wako kuwa mateka, na bidhaa yako kuwa mawindo; nao watazibomoa kuta zako, na kuziharibu nyumba zako zipendezazo; nao wataweka mawe yako, na miti yako, na mavumbi yako, kati ya maji. |
13. | Nami nitaikomesha sauti ya nyimbo zako, wala sauti ya vinubi vyako haitasikiwa tena. |
14. | Nami nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi; hutajengwa tena; maana mimi, Bwana, nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU. |
15. | Bwana MUNGU amwambia Tiro neno hili; Je! Visiwa havitatikisika kwa mshindo wa kuanguka kwako, watakapougua waliojeruhiwa, yatakapofanyika machinjo kati yako. |
16. | Ndipo wakuu wote wa bahari watashuka kutoka viti vyao vya enzi, na kuweka upande mavazi yao, na kuvua nguo zao zilizotiwa taraza; watajivika matetemeko; wataketi na kutetemeka kila dakika, na kukustaajabia, |
17. | Nao watakufanyia maombolezo, na kukuambia, Imekuwaje wewe kuharibika, wewe uliyekaliwa na wana-maji, mji wenye sifa, uliyekuwa na nguvu katika bahari, mji huo, na hao waliokaa ndani yake, waliowatia hofu wote waliokaa ndani yake! |
18. | Sasa visiwa vitatetemeka katika siku ya kuanguka kwako; naam, visiwa vilivyo katika bahari vitafadhaika, kwa sababu ya kuondoka kwako. |
19. | Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokufanya kuwa mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa na watu; nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako, na maji makuu yatakapokufunika; |
20. | ndipo nitakapokushusha pamoja nao washukao shimoni, uende kwa watu wa kale; nami nitakukalisha pande za chini za nchi; mahali palipokuwa ukiwa tangu zamani, pamoja nao washukao shimoni; ili usikaliwe na watu, wala usiweke utukufu wako katika nchi yao walio hai. |
21. | Nitakufanya kuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwako tena; ujapotafutwa, lakini hutaonekana tena kabisa, asema Bwana MUNGU. |
← Ezekiel (26/48) → |