Ezekiel (25/48)  

1. Neno la Bwana likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, uwaelekezee wana wa Amoni uso wako, ukatabiri juu yao.
3. Uwaambie hao wana wa Amoni, Lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umesema, Aha! Juu ya patakatifu pangu, palipotiwa unajisi; na juu ya nchi ya Israeli, ilipoharibiwa; na juu ya nyumba ya Israeli, walipokwenda kifungoni;
4. basi, kwa sababu hiyo, nitakutia katika mikono ya wana wa mashariki uwe milki yao, nao wataweka marago yao ndani yako, kufanya maskani zao ndani yako; watakula matunda yako, na kunywa maziwa yako.
5. Nami nitafanya Raba kuwa banda la ngamia, na wana wa Amoni kuwa mahali pa kulaza makundi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
6. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umepiga makofi, na kupiga mshindo kwa miguu yako, na kufurahi juu ya nchi ya Israeli, jeuri yote ya roho yako;
7. basi, tazama, nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nitakutoa uwe mateka ya mataifa; nami nitakukatilia mbali na kabila za watu, nami nitakuangamiza, usiwe katika nchi hizo; nitakukomesha; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
8. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu Moabu na Seiri husema, Tazama, nyumba ya Israeli ni sawasawa na mataifa yote;
9. basi, tazama, nitawafunulia wana wa mashariki ubavu wa Moabu toka miji yake, toka miji yake iliyo mipakani mwake, utukufu wa nchi hiyo, Beth-yeshimothi, na Baal-meoni, na Kiriathaimu,
10. pamoja na wana wa Amoni, nami nitawatoa kuwa milki, ili wana wa Amoni wasikumbukwe kati ya mataifa,
11. nami nitatoa hukumu juu ya Moabu; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
12. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Edomu wametenda kinyume cha nyumba ya Yuda, kwa kujilipiza kisasi, nao wamekosa sana, na kujilipiza kisasi juu yao;
13. kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Nitanyosha mkono wangu juu ya Edomu, nitakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama; nami nitaifanya kuwa ukiwa toka Temani; na mpaka Dedani wataanguka kwa upanga.
14. Nami nitaweka kisasi changu juu ya Edomu, kwa mkono wa watu wangu Israeli; nao watatenda mambo katika Edomu, kwa kadiri ya hasira yangu, na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana MUNGU.
15. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Wafilisti wametenda mambo kwa kujilipiza kisasi, nao wamejilipiza kisasi kwa jeuri ya roho, ili kupaangamiza kwa uadui wa daima;
16. kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitanyosha mkono wangu juu ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi, na kuwaharibu wabakio pande za pwani.
17. Nami nitajilipiza kisasi kikuu, nikiwakemea kwa ukali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapojilipiza kisasi juu yao.

  Ezekiel (25/48)