← Ezekiel (23/48) → |
1. | Neno la Bwana likanijia tena, kusema, |
2. | Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja; |
3. | nao walizini huko Misri; walizini wakati wa ujana wao; huko vifua vyao vililemewa, na huko waliyabana matiti ya ubikira wao. |
4. | Na majina yao, mkubwa aliitwa Ohola, na umbu lake Oholiba; wakawa wangu, wakazaa wana na binti. Na katika hayo majina yao, Samaria ni Ohola, na Yerusalemu ni Oholiba. |
5. | Na Ohola alifanya mambo ya kikahaba alipokuwa wangu; naye alipenda mno wapenzi wake, Waashuri, jirani zake, |
6. | waliovikwa samawi, maliwali na mawaziri, wote vijana wa kutamanika, wapanda farasi wakipanda farasi zao. |
7. | Akawagawia mambo yake ya kikahaba, watu wateule wa Ashuru, wote pia; akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mmoja wa hao aliowapenda. |
8. | Wala hakuyaacha mambo yake ya kikahaba tangu siku za Misri, kwa maana wakati wa ujana wake walilala naye, wakayabana matiti ya ubikira wake wakamwaga uzinzi wao juu yake. |
9. | Kwa sababu hiyo nalimtia katika mikono ya wapenzi wake, katika mikono ya Waashuri, aliowapendelea. |
10. | Na hawa wakaufunua uchi wake, wakatwaa wanawe na binti zake, wakamwua yeye kwa upanga; akawa jina la aibu kati ya wanawake; kwa maana walitoa hukumu juu yake. |
11. | Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake. |
12. | Aliwapendelea Waashuri, maliwali na mawaziri, jirani zake, waliovikwa nguo za shani, wapanda farasi wakipanda farasi zao, wote pia vijana wa kutamanika. |
13. | Nikaona ya kuwa ametiwa unajisi; wote wawili walifuata njia moja. |
14. | Naye akaongeza uzinzi wake; kwa maana aliona watu waume, ambao sura zao zimeandikwa ukutani, sura za Wakaldayo zilizoandikwa kwa rangi nyekundu; |
15. | waliofungiwa mikumbuu viunoni mwao, na vilemba vilivyotiwa rangi vichwani mwao; wote wakuu wa kuangaliwa, kwa mfano wa wana wa Babeli katika Ukaldayo, katika nchi ya kuzaliwa kwao. |
16. | Na mara alipowaona aliwapendelea, akatuma wajumbe kwao hata Ukaldayo. |
17. | Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao. |
18. | Basi alifunua uzinzi wake, na kufunua uchi wake; ndipo roho yangu ikafarakana naye, kama ilivyofarakana na umbu lake. |
19. | Lakini aliongeza uzinzi wake, akikumbuka siku za ujana wake, alipofanya mambo ya kikahaba katika nchi ya Misri. |
20. | Akawapendelea wapenzi wao, ambao nyama ya mwili wao ni kama nyama ya mwili wa punda, nacho kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. |
21. | Ndivyo ulivyokumbuka uasherati wa ujana wako, yalipobanwa matiti yako na Wamisri, kwa maziwa ya ujana wako. |
22. | Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainua wapenzi wako juu yako, ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote; |
23. | watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, maliwali na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi. |
24. | Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu sawasawa na hukumu zao. |
25. | Nami nitaweka wivu wangu juu yako, nao watakutenda mambo kwa ghadhabu; watakuondolea pua yako na masikio yako; na mabaki yako wataanguka kwa, upanga; watawatwaa wanao na binti zako; na mabaki yako watateketea motoni. |
26. | Pia watakuvua nguo zako, na kukuondolea vyombo vyako vya uzuri. |
27. | Hivyo ndivyo nitakavyoukomesha uasherati wako, na uzinzi wako, ulioletwa toka nchi ya Misri; usije ukawainulia macho yako, na kukumbuka Misri tena. |
28. | Maana Bwana MUNGU asema hivi, Tazama nitakutia katika mikono yao unaowachukia, katika mikono yao, ambao roho imefarakana nao; |
29. | nao watakutenda mambo kwa chuki, watakuondolea kazi zako zote, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako. |
30. | Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao. |
31. | Umekwenda katika njia ya umbu lako; basi nitatia kikombe chake katika mkono wako. |
32. | Bwana MUNGU asema hivi; Utakinywea kikombe cha umbu lako; chenye nafasi nyingi kikubwa; utadhihakiwa na kudharauliwa; kimejaa sana. |
33. | Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha umbu lako Samaria. |
34. | Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili. |
35. | Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako. |
36. | Tena Bwana akaniambia, Mwanadamu, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi uwahubiri machukizo yao. |
37. | Maana wamezini, na damu imo mikononi mwao, nao wamezini na vinyago vyao; tena wana wao walionizalia wamewapitisha katika moto ili waliwe nao. |
38. | Tena wamenitenda haya; wamepatia unajisi mahali pangu patakatifu, siku ile ile, nao wamezitangua sabato zangu. |
39. | Kwa maana walipokuwa wamekwisha kuvichinjia vinyago vyao watoto wao, ndipo walipoingia patakatifu pangu, siku ile ile, wapatie unajisi, na tazama, wamefanya hivyo kati ya nyumba yangu. |
40. | Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kujipamba vyombo vya uzuri; |
41. | ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu. |
42. | Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji nzuri juu ya vichwa vyao. |
43. | Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye! |
44. | Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati. |
45. | Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu. |
46. | Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitaleta kusanyiko la watu juu yao, nami nitawatoa warushwe huko na huko, na kutekwa nyara. |
47. | Na kusanyiko hilo watawapiga kwa mawe, na kuwaua kwa panga zao; watawaua wana wao na binti zao, na kuziteketeza nyumba zao kwa moto. |
48. | Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi hii, ili wanawake wote wafundishwe, wasifanye mambo ya uasherati wenu. |
49. | Nao watawalipa ninyi malipo ya uasherati wenu, nanyi mtachukua dhambi za vinyago vyenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU. |
← Ezekiel (23/48) → |