← Ezekiel (21/48) → |
1. | Neno la Bwana likanijia, kusema, |
2. | Mwanadamu, uelekeze uso wako kuelekea Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli; |
3. | uiambie nchi ya Israeli, Bwana asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya. |
4. | Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hata kaskazini, |
5. | na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena. |
6. | Ugua, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika kwake viuno vyako, na kwa uchungu, utaugua mbele ya macho yao. |
7. | Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unaugua? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatalegea kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU. |
8. | Neno la Bwana likanijia, kusema, |
9. | Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa, |
10. | umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti. |
11. | Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye. |
12. | Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani. |
13. | Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU. |
14. | Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote. |
15. | Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje. |
16. | Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako. |
17. | Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, Bwana, nimenena neno hili. |
18. | Neno la Bwana likanijia tena, kusema, |
19. | Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. |
20. | Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. |
21. | Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. |
22. | Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. |
23. | Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. |
24. | Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono. |
25. | Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho; |
26. | Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. |
27. | Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa. |
28. | Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari za wana wa Amoni, na katika habari za aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umesuguliwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme; |
29. | wakati wakuoneapo ubatili, wakati wakufanyiao uganga wa uongo, ili kukuweka juu ya shingo zao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho. |
30. | Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe. |
31. | Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza. |
32. | Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itakuwa katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, Bwana, nimenena neno hili. |
← Ezekiel (21/48) → |