← Ezekiel (19/48) → |
1. | Tena uwaombolezee wakuu wa Israeli, |
2. | useme, Mama yako alikuwa nini? Simba mke; alijilaza kati ya simba, kati ya wana-simba aliwalisha watoto wake. |
3. | Akamlea mtoto mmoja katika watoto wake, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu. |
4. | Mataifa nao wakapata habari zake, akanaswa katika rima lao, wakamchukua kwa kulabu mpaka nchi ya Misri. |
5. | Basi mamaye alipoona kwamba amemngoja, na tumaini lake limepotea, akatwaa mtoto mwingine katika watoto wake, akamfanya mwana-simba. |
6. | Naye akaenda huko na huko kati ya simba, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu. |
7. | Akayajua majumba yao, akaiharibu miji yao; nchi ikawa ukiwa, navyo vitu vilivyoijaza, kwa sababu ya mshindo wa kunguruma kwake. |
8. | Ndipo mataifa wakajipanga juu yake pande zote toka nchi zote; wakaunda wavu wao juu yake; akanaswa katika rima lao. |
9. | Wakamtia katika tundu kwa kulabu, wakamleta kwa mfalme wa Babeli wakamtia ndani ya ngome, sauti yake isisikiwe tena juu ya milima ya Israeli. |
10. | Mama yako alikuwa kama mzabibu, katika damu yako, uliopandwa karibu na maji; akazaa sana na kujaa matawi, kwa sababu ya maji mengi. |
11. | Naye alikuwa na vijiti vya nguvu, kwa fimbo za enzi zao watawalao, na kimo chao kiliinuka kati ya matawi manene, wakaonekana kwa urefu wao, pamoja na wingi wa matawi yao. |
12. | Lakini aling'olewa kwa ghadhabu, akaangushwa chini, upepo wa mashariki ukakausha matunda yake; vijiti vyake vya nguvu vikavunjika, vikakauka; moto ulivila. |
13. | Na sasa umepandwa jangwani, katika nchi kavu, ya ukame. |
14. | Na moto umetoka katika vijiti vya matawi yake, umekula matunda yake, hata hana tena kijiti cha nguvu kifaacho kwa fimbo ya enzi ya kutawala. Na hayo ni maombolezo, nayo yatakuwa maombolezo. |
← Ezekiel (19/48) → |