Ezekiel (16/48)  

1. Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2. Mwanadamu, uujulishe Yerusalemu machukizo yake,
3. useme, Bwana MUNGU auambia Yerusalemu hivi; Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti.
4. Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa.
5. Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa.
6. Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai.
7. Nalikufanya kuwa maelfu-elfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, huna nguo.
8. Basi, nilipopita karibu nawe, nikakutazama; tazama, wakati wako ulikuwa wakati wa upendo; nikatandika upindo wa vazi langu juu yako, nikakufunika uchi wako; naam, nalikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu.
9. Kisha nikakuosha kwa maji; naam, nalikuosha kabisa damu yako, nikakupaka mafuta;
10. nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa hariri.
11. Nikakupamba kwa mapambo pia, nikatia vikuku mikononi mwako, na mkufu shingoni mwako.
12. Nikatia hazama puani mwako, na pete masikioni mwako, na taji nzuri juu ya kichwa chako.
13. Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; na mavazi yako yalikuwa ya kitani safi, na hariri, na kazi ya taraza; ulikula unga mzuri, na asali, na mafuta; nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikilia hali ya kifalme.
14. Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU.
15. Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako, ukamwaga mambo yako ya kikahaba juu ya kila mtu aliyepita; ulikuwa wake.
16. Ukatwaa baadhi ya mavazi yako, ukajifanyia mahali palipoinuka, palipopambwa kwa rangi mbalimbali, ukafanya mambo ya kikahaba juu yake; mambo kama hayo hayatakuja wala hayatakuwako.
17. Pia ulivitwaa vyombo vyako vya uzuri, vya dhahabu yangu na vya fedha yangu, nilivyokupa, ukajifanyia sanamu za wanaume, ukafanya mambo ya kikahaba pamoja nazo;
18. ukatwaa nguo zako za kazi ya taraza, ukawafunika, ukaweka mafuta yangu na uvumba wangu mbele yao.
19. Mkate wangu niliokupa, unga mzuri, na mafuta, na asali, nilivyokulisha, ukaviweka mbele yao viwe harufu ya kupendeza; na ndivyo vilivyokuwa; asema Bwana MUNGU.
20. Pamoja na hayo uliwatwaa wana wako na binti zako, ulionizalia, ukawatoa sadaka kwao ili waliwe. Je! Mambo yako ya kikahaba ni kitu kidogo tu,
21. hata ukawaua watoto wangu, na kuwatoa kwa kuwapitisha motoni kwa hao?
22. Na katika machukizo yako yote, na mambo yako ya kikahaba, hukuzikumbuka siku za ujana wako, ulipokuwa uchi, huna nguo, ukawa ukigaagaa katika damu yako.
23. Tena, imekuwa baada ya uovu wako wote, (ole wako! ole wako! Asema Bwana MUNGU,)
24. ulijijengea mahali palipoinuka, ukajifanyia mahali palipoinuka katika kila njia kuu.
25. Umejenga mahali pako palipoinuka penye kichwa cha kila njia, ukaufanya uzuri wako kuwa chukizo, ukatanua miguu yako kwa kila mtu aliyepita karibu, ukaongeza mambo yako ya kikahaba.
26. Tena umezini na Wamisri, jirani zako, wakuu wa mwili; ukaongeza mambo yako ya kikahaba, ili kunikasirisha.
27. Basi, tazama, kwa ajili ya hayo nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nimelipunguza posho lako, na kukutoa kwa mapenzi yao wanaokuchukia, binti za Wafilisti, walioyaonea haya mambo yako ya uasherati.
28. Pia umefanya mambo ya kikahaba pamoja na Waashuri, kwa sababu ulikuwa huwezi kushibishwa; naam, umefanya mambo ya kikahaba pamoja nao, wala hujashiba bado.
29. Pamoja na hayo umeongeza mambo yako ya kikahaba katika nchi ya Kanaani, mpaka Ukaldayo, wala hujashibishwa kwa hayo.
30. Jinsi moyo wako ulivyokuwa dhaifu, asema Bwana MUNGU, ikiwa unafanya mambo hayo yote, kazi ya mwanamke mzinzi,
31. apendaye kutawala watu; kwa kuwa wajijengea mahali pako pakuu penye kichwa cha kila njia, na kufanya mahali pako palipoinuka katika kila njia kuu; lakini hukuwa kama kahaba, kwa maana ulidharau kupokea ujira.
32. Mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!
33. Watu huwapa makahaba wote zawadi, bali wewe unawapa wapenzi wako wote zawadi zako, na kuwapa rushwa ili waje kwako pande zote, kwa ajili ya mambo yako ya kikahaba.
34. Tena, katika mambo yako ya kikahaba, wewe na wanawake wengine ni mbalimbali, kwa kuwa hapana akufuataye katika mambo yako ya kikahaba; tena kwa kuwa unatoa ujira, wala hupewi ujira; basi, njia yako na njia yao ni mbalimbali.
35. Kwa sababu hiyo, Ewe kahaba, lisikie neno la Bwana;
36. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu uchafu wako umemwagwa, na uchi wako umefunuliwa, kwa njia ya uzinzi wako pamoja na wapenzi wako; na kwa sababu ya vinyago vyote vya machukizo yako; na kwa sababu ya damu ya watoto wako, uliyowapa;
37. basi, tazama, nitawakusanya wapenzi wako wote ambao umejifurahisha pamoja nao, nao wote uliowapenda, pamoja na watu wote uliowachukia; naam, nitawakusanya juu yako pande zote, na kuwafunulia uchi wako, wapate kuuona uchi wako wote.
38. Nami nitakuhukumu, kama wahukumiwavyo wake walioolewa wazinio, na kumwaga damu, nami nitakupatiliza damu ya ghadhabu na wivu.
39. Tena nitakutia katika mikono yao, nao watapaangusha mahali pako pakuu, na kupabomoa mahali pako palipoinuka, nao watakuvua nguo zako, na kutwaa vyombo vyako vya uzuri, nao watakuacha uchi, huna nguo.
40. Tena wataleta mkutano wa watu juu yako, nao watakupiga kwa mawe, na kukuchoma kwa panga zao.
41. Nao watazipiga moto nyumba zako, na kutekeleza hukumu juu yako mbele ya wanawake wengi, nami nitakulazimisha kuacha mambo ya kikahaba, wala hutatoa ujira tena.
42. Hivyo ndivyo nitakavyoshibisha ghadhabu yangu juu yako, na wivu wangu utanitoka, nami nitatulia wala sitaona hasira tena.
43. Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, bali umenikasirisha kwa mambo hayo yote; basi, tazama, mimi nami nitaleta njia yako juu ya kichwa chako, asema Bwana MUNGU; wala hutafanya uasherati zaidi ya machukizo yako yote.
44. Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.
45. Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.
46. Na umbu lako mkubwa ni Samaria, akaaye mkono wako wa kushoto, yeye na binti zake; na umbu lako mdogo, akaaye mkono wako wa kuume, ni Sodoma na binti zake.
47. Lakini hukuenda katika njia zao, wala hukutenda sawasawa na machukizo yao; lakini kana kwamba hilo ni jambo dogo sana, ulikuwa umeharibika kuliko wao katika njia zako zote.
48. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, Sodoma, umbu lako, yeye na binti zake, hawakutenda kama wewe ulivyotenda, wewe na binti zako.
49. Tazama, uovu wa umbu lako, Sodoma, ulikuwa huu; kiburi, na kushiba chakula, na kufanikiwa, hayo yalikuwa ndani yake na binti zake; tena hakuutia nguvu mkono wa maskini na mhitaji.
50. Nao walijivuna, wakafanya machukizo mbele zangu; kwa sababu hiyo naliwaondoa hapo nilipoyaona.
51. Samaria naye hakutenda nusu ya dhambi zako; bali wewe umeyaongeza machukizo yako zaidi ya hao, nawe umewapa haki maumbu yako kwa machukizo yako yote uliyoyatenda.
52. Wewe nawe, ichukue aibu yako mwenyewe, kwa kuwa umetoa hukumu juu ya maumbu yako; kwa dhambi zako ulizozitenda, zilizochukiza kuliko hao, wao wana haki kuliko wewe; naam, ufedheheke wewe nawe, ukaichukue aibu yako, kwa kuwa umewapa haki maumbu yako.
53. Nami nitawarudisha watu wao waliofungwa; wafungwa wa Sodoma na binti zake, na wafungwa wa Samaria na binti zake na wafungwa wako waliofungwa kati yao;
54. upate kuichukua aibu yako mwenyewe, na kutahayari, kwa sababu ya mambo yote uliyoyatenda, kwa kuwa umekuwa faraja kwao.
55. Na maumbu yako, Sodoma na binti zake, watairudia hali yao ya kwanza, na Samaria na binti zake watairudia hali yao ya kwanza, na wewe na binti zako mtairudia hali yenu ya kwanza.
56. Kwa maana umbu lako, Sodoma, hakutajwa kwa kinywa chako katika siku ya kiburi chako;
57. kabla uovu wako haujafunuliwa bado, kama vile wakati ule walipokutukana binti za Shamu, na wale wote waliomzunguka, binti za Wafilisti wanaokudharau pande zote.
58. Umeuchukua uasherati wako, na machukizo yako, asema Bwana.
59. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano.
60. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe.
61. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako.
62. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana;
63. upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU.

  Ezekiel (16/48)