← Ezekiel (12/48) → |
1. | Neno la Bwana likanijia tena, kusema, |
2. | Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. |
3. | Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi. |
4. | Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watokavyo katika kuhamishwa. |
5. | Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale. |
6. | Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi; kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli. |
7. | Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nalitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao. |
8. | Asubuhi neno la Bwana likanijia, kusema, |
9. | Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, Unafanya nini wewe? |
10. | Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao. |
11. | Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa. |
12. | Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake. |
13. | Tena wavu wangu nitautandika juu yake, naye atanaswa kwa mtego wangu; nami nitampeleka Babeli, mpaka nchi ya Wakaldayo; lakini hataiona, angawa atakufa huko. |
14. | Nami nitawatawanya kwa pepo zote wote wamzungukao ili wamsaidie, na vikosi vyake vyote; nami nitaufuta upanga nyuma yao. |
15. | Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatupa-tupa katika nchi zote. |
16. | Lakini nitawasaza watu wachache miongoni mwao na kuwaokoa na upanga, na njaa, na tauni ili watangaze habari ya machukizo yao yote, kati ya mataifa huko waendako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
17. | Tena neno la Bwana likanijia, kusema, |
18. | Mwanadamu, ule chakula chako kwa matetemo, ukanywe maji yako kwa kutetemeka na kwa kuyatunza sana; |
19. | ukawaambie watu wa nchi, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari zao wakaao Yerusalemu, na katika nchi ya Israeli; Watakula chakula chao kwa kukitunza sana, na maji yao watayanywa kwa ushangao, nchi yao iwe ukiwa, kwa kukosa vitu vyote viijazavyo, kwa sababu ya udhalimu wao wote wakaao ndani yake. |
20. | Na miji yote yenye watu itakuwa maganjo, nayo nchi itakuwa ukiwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. |
21. | Neno la Bwana likanijia, kusema, |
22. | Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi. |
23. | Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote. |
24. | Kwa maana hayatakuwapo tena maono yo yote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli. |
25. | Maana mimi ni Bwana; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU. |
26. | Neno la Bwana likanijia tena, kusema, |
27. | Mwanadamu, tazama, hao wa nyumba ya Israeli husema, Maono hayo ayaonayo ni ya siku nyingi zijazo, naye anatabiri habari ya nyakati zilizo mbali sana. |
28. | Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Maneno yangu hayatakawilishwa tena hata moja, bali neno nitakalolinena litatimizwa, asema Bwana MUNGU. |
← Ezekiel (12/48) → |