Ezekiel (11/48)  

1. Tena roho ikaniinua, ikanileta hata lango la upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana, lililoelekea upande wa mashariki; na tazama, mahali pa kuingilia pa lango walikuwako watu ishirini na watano; na katikati yao nikamwona Yaazania, mwana wa Azuri, na Pelatia, mwana wa Benaya, nao ni wakuu wa watu.
2. Akaniambia, Mwanadamu, hawa ndio watu wale watungao uovu, na kutoa mashauri mabaya ndani ya mji huu;
3. wasemao, Wakati wa kujenga nyumba si karibu; mji huu ni sufuria na sisi ni nyama.
4. Basi toa unabii juu yao, Ee mwanadamu, toa unabii.
5. Roho ya Bwana ikaniangukia, naye akaniambia, Nena, Bwana asema hivi; Mmesema maneno hayo, Enyi nyumba ya Israeli; maana mimi nayajua yaingiayo katika mioyo yenu.
6. Mmewaongeza watu wenu waliouawa ndani ya mji wenu, nanyi mmezijaza njia kuu zake waliouawa.
7. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Watu wenu waliouawa, ambao mmewalaza katikati yake, hao ndio nyama hiyo, na mji huu ndio sufuria; lakini ninyi mtatolewa nje kutoka katikati yake.
8. Ninyi mmeuogopa upanga; nami nitauleta upanga juu yenu, asema Bwana MUNGU.
9. Nami nitawatoa ninyi nje kutoka katikati yake, na kuwatia katika mikono ya wageni, nami nitafanya hukumu kati yenu.
10. Mtaanguka kwa upanga; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
11. Mji huu hautakuwa sufuria lenu, wala ninyi hamtakuwa nyama ndani yake; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli;
12. nanyi mtajua ya kuwa mimi ni Bwana; kwa maana hamuendi katika amri zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, bali mmetenda mambo kama hukumu za mataifa wanaowazunguka.
13. Ikawa, nilipotoa unabii, Pelatia, mwana wa Benaya, akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu, nikasema, Ee Bwana MUNGU, je! Utawakomesha kabisa mabaki ya Israeli?
14. Neno la Bwana likanijia, kusema,
15. Mwanadamu, ndugu zako, naam, ndugu zako, watu wa jamaa zako, na nyumba yote ya Israeli, wote pia, ndio hao ambao wenyeji wa Yerusalemu wamewaambia, Jitengeni mbali na Bwana, nchi hii tumepewa sisi, iwe milki yetu;
16. basi nena, Bwana MUNGU asema hivi, Ikiwa mimi nimewahamisha, wakae katika mataifa, na ikiwa mimi nimewatawanya katika nchi kadha wa kadha, pamoja na hayo nitakuwa patakatifu kwao kwa muda mchache, katika nchi zile walizozifikilia.
17. Basi nena, Bwana MUNGU asema hivi; Nitawakusanya ninyi toka kati ya kabila za watu, na kuwakutanisha toka nchi zile mlizotawanyika, nami nitawapeni nchi ya Israeli.
18. Nao watafika huko, nao wataondolea mbali vitu vyake vyote vichukizavyo, na machukizo yake yote.
19. Nami nitawapa moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa kijiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama;
20. ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
21. Bali wao ambao mioyo yao huenda kwa kuufuata moyo wa vitu vyao vichukizavyo, na machukizo yao, nitaileta njia yao iwajilie juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.
22. Ndipo hao makerubi wakainua mabawa yao, nayo magurudumu yalikuwa karibu nao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
23. Utukufu wa Bwana ukapaa juu toka katikati ya mji, ukasimama juu ya mlima wa upande wa mashariki wa mji.
24. Na roho hiyo ikaniinua, ikanichukua katika maono, kwa nguvu za roho ya Mungu, hata Ukaldayo, kwa watu wale wa uhamisho. Basi maono niliyoyaona yakaniacha.
25. Ndipo nikawaambia watu wa uhamisho habari ya mambo yote aliyonionyesha Bwana.

  Ezekiel (11/48)