Exodus (38/40)  

1. Kisha akafanya hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ya mti wa mshita urefu wake ulikuwa dhiraa tano, na upana wake ulikuwa dhiraa tano, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa dhiraa tatu.
2. Naye akazifanya pembe zake katika ncha zake nne; hizo pembe zilikuwa za kitu kimoja nayo; naye akaifunika shaba.
3. Kisha akafanya vyombo vyote vya madhabahu, yaani sufuria zake, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote akavifanya vya shaba.
4. Naye akaifanyia madhabahu wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo kuizunguka pande zote, ukawa katikati ya hiyo madhabahu.
5. Naye akasubu vikuku vinne kwa kutiwa katika pembe nne za huo wavu wa shaba, viwe mahali pa kutia ile miti ya kuichukulia.
6. Naye akaifanya hiyo miti kwa mti wa mshita na kuifunika shaba.
7. Naye akaitia ile miti katika vile vikuku vilivyokuwa katika mbavu za hiyo madhabahu, ili kuichukua; akaifanya yenye mvungu ndani, kwa zile mbao.
8. Kisha akafanya hilo birika la shaba, na tako lake la shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania.
9. Naye akafanya ule ua; upande wa kusini kwa kuelekea kusini, chandarua ya ua ilikuwa ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kiasi cha dhiraa mia;
10. nguzo zake zilikuwa ishirini, na matako yake yalikuwa ishirini, yalikuwa ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
11. Upande wa kaskazini ulikuwa ni dhiraa mia vivyo, nguzo zake ishirini na matako yake ishirini, yalikuwa ni ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
12. Upande wa magharibi mlikuwa na chandarua ya dhiraa hamsini, nguzo zake zilikuwa ni kumi, na matako yake kumi; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
13. Upande wa mashariki kuelekea mashariki dhiraa hamsini.
14. Chandarua ya upande mmoja wa lango ilikuwa dhiraa kumi na tano urefu wake; na nguzo zake tatu, na matako yake matatu;
15. ni vivyo upande wa pili; upande huu na huu langoni mwa ua mlikuwa na chandarua ya dhiraa kumi na tano urefu wake; nguzo zake zilikuwa ni tatu, na matako yake matatu.
16. Chandarua za nguo zote za ule ua zilizouzunguka pande zote zilikuwa za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa.
17. Na matako ya zile nguzo yalikuwa ya shaba; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha; na vichwa vya zile nguzo vilikuwa ni vya fedha; na nguzo zote za huo ua ziliungwa kwa vitanzi vya fedha.
18. Na hilo pazia la lango la ua, lilikuwa ni kazi ya mwenye kutia taraza, lilikuwa la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; lilikuwa na urefu wake dhiraa ishirini, na kutukuka kwake katika huo upana wake kulikuwa dhiraa tano, kupatana na ile chandarua ya ua.
19. Na nguzo zake zilikuwa nne, na matako yake manne, yalikuwa ya shaba; kulabu zake zilikuwa za fedha, na vichwa vyake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
20. Na vigungi vyote vya maskani, na vya ua ulioizunguka pande zote vilikuwa vya shaba.
21. Jumla ya vile vyombo vilivyofanywa kwa ajili ya hiyo maskani, hiyo maskani ya ushuhuda ni hii, kama vilivyohesabiwa, kama maagizo ya Musa yalivyokuwa, kwa ajili ya utumishi wa Walawi kwa mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni, kuhani.
22. Na Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda, akafanya yote Bwana aliyomwagiza Musa.
23. Na pamoja naye alikuwa na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani, aliyekuwa fundi wa kuchora nakshi, mfanyaji wa kazi mwerevu, naye alikuwa mwenye kutia taraza za nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri.
24. Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya hiyo kazi, katika kazi hiyo yote ya mahali patakatifu, hiyo dhahabu ya matoleo, ilikuwa ni talanta ishirini na kenda, na shekeli mia saba na thelathini, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu.
25. Na fedha ya hao waliohesabiwa, watu wa huo mkutano ilikuwa talanta mia, na shekeli elfu moja na mia saba na sabini na tano kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu;
26. kichwa beka, maana, nusu shekeli, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu, kwa ajili ya kila mtu aliyepita kwa wale waliohesabiwa, aliyekuwa wa umri wa miaka ishirini au zaidi, kwa ajili ya watu waume sita mia na tatu elfu, na mia tano na hamsini (603,550).
27. Na hizo talanta mia za fedha zilikuwa kwa kusubu yale matako ya mahali patakatifu na matako ya hilo pazia; matako mia kwa hizo talanta mia, talanta moja tako moja.
28. Na kwa hizo shekeli elfu moja na mia saba, na sabini na tano, akafanya vifungo vya hizo nguzo, na kuvifunika fedha vile vichwa vyake, na kufanya vitanzi vyake.
29. Na hiyo shaba iliyoletwa ilikuwa ni talanta sabini, na shekeli elfu mbili na mia nne.
30. Naye akafanya ya hiyo shaba matako kwa ajili ya lango la hema ya kukutania, na hiyo madhabahu ya shaba, na ule wavu wa shaba kwa ajili yake na vyombo vyote vya hiyo madhabahu,
31. na matako ya ua kuuzunguka pande zote, na matako ya lango la huo ua, na vigingi vyote vya maskani, na vigingi vyote vya huo ua uliozunguka pande zote.

  Exodus (38/40)