← Exodus (35/40) → |
1. | Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia Bwana ni haya, kwamba myafanye. |
2. | Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa. |
3. | Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato. |
4. | Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema, |
5. | Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba; |
6. | na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi; |
7. | na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na mbao za mshita; |
8. | na mafuta kwa hiyo taa, na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri; |
9. | na vito vya shohamu, na vito vya kutiwa kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani. |
10. | Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo Bwana ameyaagiza; |
11. | yaani, hiyo maskani na hema yake, na kifuniko chake, na vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na viguzo vyake, na matako yake; |
12. | hilo sanduku, na miti yake, na hicho kiti cha rehema, na lile pazia la sitara; |
13. | na hiyo meza, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hiyo mikate ya wonyesho; |
14. | na hicho kinara cha taa kwa mwanga, na vyombo vyake, na taa zake, na hayo mafuta kwa nuru; |
15. | na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, na miti yake, na hayo mafuta ya kupaka, na huo uvumba mzuri, na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; |
16. | na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hilo birika na tako lake; |
17. | na hizo kuta za nguo za ua, na viguzo vyake, na matako yake, na pazia la lango la ua; |
18. | na vile vigingi vya maskani, na vigingi vya ua, na kamba zake |
19. | na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani. |
20. | Basi mkutano wote wa wana wa Israeli wakaondoka hapo mbele ya Musa. |
21. | Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa Bwana, kwa kazi ya hema ya kukutania, na kwa utumishi wake, na kwa hayo mavazi matakatifu. |
22. | Nao wakaja, waume kwa wake, wote waliokuwa na moyo wa kupenda, wakaleta vipini, na hazama, na pete za muhuri, na vikuku, na vyombo vyote vya dhahabu; kila mtu aliyetoa toleo la dhahabu la kumpa Bwana. |
23. | Tena kila mtu aliyeona kwake nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi, na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, akavileta. |
24. | Kila mtu aliyetoa toleo la fedha, na la shaba, akaileta sadaka ya Bwana; na kila mtu, aliyeona kwake mti wa mshita kwa kazi yo yote ya huo utumishi, akauleta. |
25. | Na wanawake wote waliokuwa na mioyo ya hekima, walisokota kwa mikono yao, nao wakaleta hizo walizokuwa wamezisokota, nguo za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na hizo nyuzi nyekundu, na hiyo nguo ya kitani nzuri. |
26. | Na wanawake wote ambao mioyo yao iliwahimiza katika hekima wakasokota hizo singa za mbuzi. |
27. | Na hao wakuu wakavileta vile vito vya shohamu, na vito vya kutiwa, kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani, |
28. | na viungo vya manukato, na mafuta; kwa hiyo taa, na kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri. |
29. | Wana wa Israeli wakaleta sadaka za kumpa Bwana kwa moyo wa kupenda; wote, waume kwa wake, ambao mioyo yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi, ambayo Bwana aliamuru ifanywe kwa mkono wa Musa. |
30. | Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; |
31. | naye amemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina; |
32. | na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, na fedha, na shaba, |
33. | na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za werevu kila aina. |
34. | Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. |
35. | Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu. |
← Exodus (35/40) → |