← Exodus (31/40) → |
1. | Bwana akanena na Musa, na kumwambia, |
2. | Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; |
3. | nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, |
4. | ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, |
5. | na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. |
6. | Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza; |
7. | yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema; |
8. | na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba; |
9. | na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake; |
10. | na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani; |
11. | na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao. |
12. | Bwana akasema na Musa, na kumwambia, |
13. | Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi. |
14. | Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. |
15. | Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa. |
16. | Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. |
17. | Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika. |
18. | Hapo Bwana alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu. |
← Exodus (31/40) → |