← Exodus (24/40) → |
1. | Kisha Bwana akamwambia Musa, Kweeni wewe, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini wa wazee wa Israeli, mkamfikilie Bwana; mkasujudie kwa mbali; |
2. | na Musa peke yake ndiye atakayekaribia karibu na Bwana; lakini hao hawatakaribia karibu; wala hao watu hawatakwea pamoja naye. |
3. | Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. |
4. | Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, |
5. | akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng'ombe. |
6. | Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. |
7. | Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. |
8. | Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote. |
9. | Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; |
10. | wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. |
11. | Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa. |
12. | Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe. |
13. | Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu. |
14. | Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na neno na awaendee. |
15. | Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima. |
16. | Na huo utukufu wa Bwana ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. |
17. | Na kuonekana kwake ule utukufu wa Bwana kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli. |
18. | Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku. |
← Exodus (24/40) → |