Exodus (20/40)  

1. Mungu akanena maneno haya yote akasema,
2. Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
3. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
5. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
6. nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
7. Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.
8. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.
9. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;
10. lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
11. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.
12. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
13. Usiue.
14. Usizini.
15. Usiibe.
16. Usimshuhudie jirani yako uongo.
17. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.
18. Watu wote wakaona umeme na ngurumo na sauti ya baragumu, na ule mlima kutoka moshi; na watu walipoona hayo wakatetemeka, wakasimama mbali.
19. Wakamwambia Musa, Sema nasi wewe, nasi tutasikia, bali Mungu asiseme nasi, tusije tukafa.
20. Musa akawaambia watu, Msiogope, maana Mungu amekuja ili awajaribu, na utisho wake uwe mbele yenu, ili kwamba msifanye dhambi.
21. Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia lile giza kuu Mungu alipokuwapo.
22. Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni.
23. Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie.
24. Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng'ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia.
25. Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi.
26. Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.

  Exodus (20/40)