Exodus (2/40)  

1. Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi.
2. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.
3. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto.
4. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata.
5. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta.
6. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.
7. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu?
8. Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto.
9. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha.
10. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.
11. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake.
12. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga.
13. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako?
14. Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.
15. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.
16. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.
17. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.
18. Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?
19. Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi.
20. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.
21. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.
22. Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni.
23. Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa.
24. Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo.
25. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.

  Exodus (2/40)