| ← Ephesians (5/6) → |
| 1. | Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; |
| 2. | mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. |
| 3. | Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; |
| 4. | wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. |
| 5. | Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. |
| 6. | Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. |
| 7. | Basi msishirikiane nao. |
| 8. | Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, |
| 9. | kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; |
| 10. | mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. |
| 11. | Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; |
| 12. | kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. |
| 13. | Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. |
| 14. | Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza. |
| 15. | Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; |
| 16. | mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. |
| 17. | Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. |
| 18. | Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; |
| 19. | mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; |
| 20. | na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo; |
| 21. | hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. |
| 22. | Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. |
| 23. | Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. |
| 24. | Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. |
| 25. | Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; |
| 26. | ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; |
| 27. | apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. |
| 28. | Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. |
| 29. | Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. |
| 30. | Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. |
| 31. | Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. |
| 32. | Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. |
| 33. | Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe. |
| ← Ephesians (5/6) → |