Ephesians (1/6)  

1. Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko [Efeso] wanaomwamini Kristo Yesu.
2. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3. Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
4. kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
5. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.
6. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.
7. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.
8. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;
9. akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo.
10. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo;
11. na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.
12. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
13. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.
14. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.
15. Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote,
16. siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu,
17. Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;
18. macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;
19. na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;
20. aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;
21. juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;
22. akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo
23. ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.

      Ephesians (1/6)