Ecclesiastes (8/12)  

1. Ni nani aliye kama mwenye hekima; Naye ni nani ajuaye kufasiri neno? Hekima ya mtu humng'ariza uso wake, Na ugumu wa uso wake hubadilika.
2. Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu.
3. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lo lote limpendezalo.
4. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini?
5. Aishikaye amri hatajua neno baya; Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu.
6. Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa;
7. kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa?
8. Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuruhusiwa katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea.
9. Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasira yake.
10. Pia nikaona waovu wamezikwa, nao wamefika kaburini; tena waliofanya mema wameondoka katika patakatifu, nao wamesahauliwa mjini. Hayo nayo ni ubatili.
11. Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya.
12. Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake;
13. walakini haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu.
14. Kuna ubatili unaofanyika juu ya nchi, kwamba wako wenye haki nao wapatilizwa kama kwa kazi yao waovu; tena wako waovu, nao wapatilizwa kama kwa kazi yao wenye haki. Nami nikasema ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
15. Kisha nikaisifu furaha, kwa sababu mwanadamu hana neno lo lote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, na kunywa, na kucheka; na yakuwa hilo likae naye katika amali yake, siku zote za maisha yake alizompa Mungu chini ya jua.
16. Mimi nilipotia moyo wangu katika kuijua hekima, na kuuona utumishi uliofanyika juu ya nchi, (maana kuna asiyepata usingizi kwa macho yake mchana wala usiku);
17. basi, niliiona kazi yote ya Mungu, ya kuwa haitafutikani na mwanadamu kazi inayofanyika chini ya jua; kwa sababu mwanadamu na akijisumbua kadiri awezavyo kuitafuta, hata hivyo hataiona; naam, zaidi ya hayo, mwenye hekima ajapodhania ya kuwa ataijua, lakini yeye hataweza kuiona.

  Ecclesiastes (8/12)