Ecclesiastes (7/12)  

1. Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.
2. Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.
3. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.
4. Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha.
5. Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu;
6. Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili.
7. Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu.
8. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.
9. Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.
10. Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo.
11. Hekima ni njema, mfano wa urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionao jua.
12. Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.
13. Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?
14. Siku ya kufanikiwa ufurahi, Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lo lote litakalofuata baada yake.
15. Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.
16. Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?
17. Usiwe mwovu kupita kiasi; Wala usiwe mpumbavu; Kwani ufe kabla ya wakati wako?
18. Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; kwa kuwa mtu yule amchaye Mungu atatoka katika hayo yote.
19. Hekima ni nguvu zake mwenye hekima, Zaidi ya wakuu kumi waliomo mjini.
20. Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.
21. Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.
22. Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine.
23. Mambo hayo yote mimi nimeyahakikisha katika hekima. Nilisema, Mimi nitakuwa na hekima, lakini imefarakana nami.
24. Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?
25. Nikageuka, na moyo wangu ulikazwa katika kujua na kupeleleza, na kuitafuta hekima, na maana ya mambo yaliyoko; ili nifahamu ya kuwa uovu ni upumbavu, na upumbavu ni wazimu.
26. Nami nimeona lililo na uchungu kupita mauti; yaani, mwanamke ambaye moyo wake ni mitego na tanzi, na mikono yake ni kama vifungo; yeye ampendezaye Mungu atamponyoka, bali mwenye dhambi atanaswa na yeye.
27. Tazama, asema Mhubiri, mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha hili na hili, ili kuitafuta jumla;
28. ambayo bado nafsi yangu nikali nikiitafuta, nisiione; mwanamume mmoja katika elfu nimemwona; bali mwanamke mmoja miongoni mwa wote mimi sikumwona.
29. Tazama, hili tu nimeliona; Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamebuni mavumbuzi mengi.

  Ecclesiastes (7/12)