Ecclesiastes (4/12)  

1. Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.
2. Kwa hiyo nikawasifu wafu waliokwisha kufa kuliko wenye uhai walio hai bado;
3. naam, zaidi ya hao wote nikamwita heri yeye asiyekuwako bado, ambaye hakuyaona mabaya yanayotendeka chini ya jua.
4. Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.
5. Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe;
6. Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu;
7. Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua.
8. Kuna mtu aliye peke yake, wala hana wa pili wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa.
9. Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.
10. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!
11. Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?
12. Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.
13. Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu.
14. Kwa maana kutoka gerezani alikuja kumiliki; naam, hata katika ufalme wake alizaliwa hali ya umaskini.
15. Nikawaona wote walio hai waendao chini ya jua, ya kwamba walishikamana na huyo kijana, huyo wa pili aliyesimama badala ya yule.
16. Hawakuwa na kikomo hao watu wote, hao wote ambao alikuwa juu yao; lakini hata hivyo wale wafuatao baada yake hawatamfurahia. Hakika hayo pia ni ubatili, na kujilisha upepo.

  Ecclesiastes (4/12)