Ecclesiastes (3/12)  

1. Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.
2. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa;
3. Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;
4. Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;
5. Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;
6. Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;
7. Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;
8. Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.
9. Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?
10. Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.
11. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.
12. Mimi najua ya kwamba hakuna jema kwao kupita kufurahi, na kufanya mema maadamu wanaishi.
13. Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.
14. Najua ya kwamba kila kazi aifanyayo Mungu itadumu milele; haiwezekani kuizidisha kitu, wala kuipunguza kitu; nayo Mungu ameifanya ili watu wamche Yeye.
15. Yale yaliyoko yamekuwako; na hayo yatakayokuwako yamekwisha kuwako; naye Mungu huyatafuta tena mambo yale yaliyopita.
16. Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu.
17. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi.
18. Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.
19. Kwa maana linalowatukia wanadamu linawatukia wanyama; jambo moja lawatukia; anavyokufa huyu ndivyo anavyokufa huyu; naam, wote wanayo pumzi moja; wala mwanadamu hana kitu cha kumpita mnyama; kwa maana yote ni ubatili.
20. Wote huendea mahali pamoja; wote hutoka katika mavumbi; na hata mavumbini hurudi tena.
21. Ni nani ajuaye kama roho ya binadamu huenda juu, na kama roho ya mnyama huenda chini?
22. Hivyo nikaona ya kwamba hakuna jema kupita mwanadamu kuzifurahia kazi zake; kwa sababu hili ni fungu lake; kwa maana ni nani atakayemrudisha tena ili ayaone yatakayomfuata baadaye.

  Ecclesiastes (3/12)