← Deuteronomy (8/34) → |
1. | Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki. |
2. | Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. |
3. | Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. |
4. | Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. |
5. | Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo. |
6. | Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha. |
7. | Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; |
8. | nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali; |
9. | nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba. |
10. | Nawe utakula ushibe, utamshukuru Bwana, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa. |
11. | Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. |
12. | Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; |
13. | na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; |
14. | basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; |
15. | aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, |
16. | aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. |
17. | Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. |
18. | Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. |
19. | Lakini itakuwa, kama ukimsahau Bwana, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka. |
20. | Kama vile mataifa yale ambayo Bwana anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya Bwana, Mungu wenu. |
← Deuteronomy (8/34) → |