| ← Deuteronomy (34/34) |
| 1. | Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. Bwana akamwonyesha nchi yote ya Gileadi hata Dani; |
| 2. | na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi; |
| 3. | na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari. |
| 4. | Bwana akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko. |
| 5. | Basi Musa, mtumishi wa Bwana, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la Bwana. |
| 6. | Akamzika bondeni, katika nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo. |
| 7. | Musa alikuwa mtu wa miaka mia na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka. |
| 8. | Wana wa Israeli wakamwombolezea Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo ya matanga ya Musa zikaisha. |
| 9. | Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa. |
| 10. | Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso; |
| 11. | katika ishara zote na maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; |
| 12. | na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote. |
| ← Deuteronomy (34/34) |