← Deuteronomy (24/34) → |
1. | Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake, kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake. |
2. | Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine. |
3. | Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha, na kumpa mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa, aliyemtwaa kuwa mkewe; |
4. | yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za Bwana; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi. |
5. | Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa. |
6. | Mtu awaye yote asitwae jiwe la kusagia, la juu wala la chini, kuwa rehani; kwani hivi ni kutwaa maisha ya mtu kuwa rehani. |
7. | Mtu akionekana anamwiba nduguze mmojawapo katika wana wa Israeli, akamfanya kama mtumwa, au kumwuza; na afe mwivi huyo; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. |
8. | Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao. |
9. | Kumbukeni na Bwana, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri. |
10. | Umkopeshapo jirani yako cho chote kikopeshwacho usiingie katika nyumba yake kwenda kutwaa rehani kwake. |
11. | Simama nje, yule umkopeshaye akuletee nje ile rehani. |
12. | Naye akiwa ni mtu maskini, usilale na rehani yake. |
13. | Sharti umrudishie rehani lichwapo jua, apate kulala na mavazi yake, na kukubarikia; nayo itakuwa ni haki kwako mbele za Bwana, Mungu wako. |
14. | Usimwonee mtumishi mwenye ujira aliye maskini na uhitaji, kama ni wa nduguzo, au kama ni wageni wako mmojawapo walio katika nchi yako, ndani ya malango yako; |
15. | mpe ujira wake kwa siku yake, wala jua lisichwe juu yake; kwa maana ni maskini, moyo wake umeutumainia huo; asije akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako. |
16. | Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe. |
17. | Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani; |
18. | bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili. |
19. | Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. |
20. | Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. |
21. | Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. |
22. | Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili. |
← Deuteronomy (24/34) → |