← Deuteronomy (19/34) → |
1. | Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na katika nyumba zao; |
2. | itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako, akupayo Bwana, Mungu wako, kuimiliki. |
3. | Itengeze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo Bwana, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko. |
4. | Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo; |
5. | kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai; |
6. | asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo. |
7. | Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu. |
8. | Na kama Bwana, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako; |
9. | nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda Bwana, Mungu wako, na kwenda sikuzote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile; |
10. | isije ikamwagika damu ya asiye makosa kati ya nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, ikawa na damu juu yako. |
11. | Lakini mtu awaye yote akimchukia mwenziwe na kumwotea na kumwinukia, akampiga hata akafa; naye akakimbilia miji hii mmojawapo; |
12. | ndipo wazee wa mji wake wapeleke ujumbe kumtwaa huko, na kumuua katika mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu, apate kufa. |
13. | Jicho lako lisimhurumie, lakini uondoe damu ya asiye makosa katika Israeli, ili upate kufanikiwa. |
14. | Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki. |
15. | Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu. |
16. | Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu ye yote na kushuhudia juu yake ya upotoe; |
17. | ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za Bwana, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo; |
18. | nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye; |
19. | ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. |
20. | Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako. |
21. | Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu. |
← Deuteronomy (19/34) → |