Daniel (2/12)  

1. Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha.
2. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme.
3. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake.
4. Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonyesha tafsiri yake.
5. Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa.
6. Bali kama mkinionyesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionyesheni ile ndoto na tafsiri yake.
7. Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonyesha tafsiri yake.
8. Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka.
9. Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionyesha tafsiri yake.
10. Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo.
11. Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili.
12. Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli.
13. Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danieli na wenzake ili wauawe.
14. Ndipo Danieli kwa busara na hadhari akamjibu Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, aliyekuwa ametoka ili kuwaua wenye hekima wa Babeli;
15. alijibu, akamwambia Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, Mbona amri hii ya mfalme ina ukali namna hii? Ndipo Arioko akamwarifu Danieli habari ile.
16. Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile.
17. Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake;
18. ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.
19. Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni.
20. Danieli akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake.
21. Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa;
22. yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake.
23. Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme.
24. Basi Danieli akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi, Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonyesha mfalme ile tafsiri.
25. Ndipo Arioko akamwingiza Danieli mbele ya mfalme kwa haraka, akamwambia hivi, Nimemwona mtu wa hao wana wa Yuda waliohamishwa, atakayemjulisha mfalme ile tafsiri.
26. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake.
27. Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu;
28. lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;
29. Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.
30. Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako.
31. Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha.
32. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba;
33. miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo.
34. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.
35. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.
36. Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.
37. Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu;
38. na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.
39. Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.
40. Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta.
41. Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope.
42. Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika.
43. Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.
44. Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.
45. Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.
46. Ndipo Nebukadreza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danieli, akatoa amri wamtolee Danieli sadaka na uvumba.
47. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii.
48. Basi mfalme akamtukuza Danieli, akampa zawadi kubwa nyingi sana, akamfanya kuwa mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na kuwa liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli.
49. Tena, Danieli akamwomba mfalme, naye akawaweka Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wawe juu ya mambo yote ya uliwali wa Babeli; lakini huyo Danieli alikuwa akiketi katika lango la mfalme.

  Daniel (2/12)