Daniel (11/12)  

1. Tena mimi, katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi, mimi nalisimama nimthibitishe na kumtia nguvu.
2. Nami sasa nitakuonyesha yaliyo kweli. Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani.
3. Na mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa mamlaka kubwa, na kutenda apendavyo.
4. Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang'olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao.
5. Na mfalme wa kusini atakuwa hodari; na mmoja wa wakuu wake atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa.
6. Na baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile.
7. Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda;
8. na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini.
9. Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe.
10. Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake.
11. Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake.
12. Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi elfu; lakini hataongezewa nguvu.
13. Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadha wa kadha, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi.
14. Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka.
15. Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga.
16. Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake.
17. Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa.
18. Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe.
19. Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
20. Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.
21. Kisha badala yake atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza.
22. Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika, naam, mkuu wa maagano pia.
23. Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo.
24. Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa wilaya hiyo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa.
25. Naye atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini hatasimama; maana watatunga hila juu yake.
26. Naam, walao sehemu ya chakula chake watamwangamiza, na jeshi lake litagharikishwa; na wengi wataanguka wameuawa.
27. Na katika habari za wafalme hao wawili, mioyo yao watanuia kutenda madhara, nao watasema uongo walipo pamoja mezani; lakini hilo halitafanikiwa; maana mwisho utatokea wakati ulioamriwa.
28. Ndipo atakaporudi mpaka nchi yake mwenye utajiri mwingi; na moyo wake utakuwa kinyume cha hilo agano takatifu; naye atafanya kama apendavyo, na kurudi mpaka nchi yake.
29. Kwa wakati ulioamriwa atarudi, na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.
30. Maana merikebu za Kitimu zitakuja kupigana naye; basi atavunjika moyo, naye atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.
31. Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, nao watalisimamisha chukizo la uharibifu.
32. Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.
33. Na hao walio wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi.
34. Basi watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo; lakini wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza.
35. Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja.
36. Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika.
37. Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote.
38. Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo.
39. Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa,
40. na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati.
41. Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni.
42. Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka.
43. Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake.
44. Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi.
45. Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia.

  Daniel (11/12)