Daniel (1/12)  

1. Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza
2. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake.
3. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;
4. vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.
5. Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
6. Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.
7. Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danieli, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego.
8. Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi.
9. Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi.
10. Mkuu wa matowashi akamwambia Danieli, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatirisha kichwa changu mbele ya mfalme.
11. Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria,
12. Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe.
13. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona.
14. Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi.
15. Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme.
16. Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.
17. Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto.
18. Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza.
19. Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme.
20. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake.
21. Tena, Danieli huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.

      Daniel (1/12)