← Amos (5/9) → |
1. | Lisikieni neno hili nilitamkalo liwe maombolezo juu yenu, enyi nyumba ya Israeli. |
2. | Bikira wa Israeli ameanguka; hatainuka tena; Ameangushwa katika nchi yake; hakuna mtu wa kumwinua. |
3. | Kwa kuwa Bwana MUNGU asema hivi; Mji uliotoka nje wenye watu elfu, utasaziwa watu mia, na mji uliotoka wenye watu mia, utasaziwa watu kumi, kwa nyumba ya Israeli. |
4. | Maana Bwana awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi; |
5. | bali msitafute Betheli, wala msiingie Gilgali, wala msipite kwenda Beer-sheba; kwani Gilgali hakika yake itakwenda utumwani, na Betheli itakuwa ubatili. |
6. | Mtafuteni Bwana, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu, nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli. |
7. | Ninyi mnaogeuza hukumu kuwa uchungu, na kuiangusha haki chini, |
8. | mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina lake; |
9. | yeye aletaye uharibifu wa ghafula juu yao walio hodari, hata uharibifu uipate ngome. |
10. | Wao humchukia yeye akemeaye langoni, nao humzira anenaye maneno ya adili. |
11. | Basi, kwa kuwa mnamkanyaga maskini, na kumtoza ngano; ninyi mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, lakini hamtakaa ndani yake; ninyi mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake. |
12. | Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao. |
13. | Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya. |
14. | Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo Bwana, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. |
15. | Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu. |
16. | Kwa ajili ya hayo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, aliye Bwana; Kutakuwako maombolezo katika njia kuu zote; nao watasema katika njia zote, Ole! Ole! Nao watamwita mkulima aje kuombolea, na hao walio hodari wa kulia waje kuomboleza. |
17. | Tena katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwako kulia; kwa maana mimi nitapita katikati yako, asema Bwana. |
18. | Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru. |
19. | Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. |
20. | Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga. |
21. | Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. |
22. | Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. |
23. | Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. |
24. | Lakini hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu. |
25. | Je! Mliniletea dhabihu na sadaka jangwani muda wa miaka arobaini, enyi nyumba ya Israeli? |
26. | Naam, mtamchukua Sikuthi, mfalme wenu, na Kiuni, sanamu zenu, nyota ya mungu wenu, mliojifanyizia wenyewe. |
27. | Kwa sababu hiyo nitawahamisha, hali ya kufungwa, mwende mbali kupita Dameski, asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi. |
← Amos (5/9) → |