Amos (2/9)  

1. Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Moabu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu aliichoma moto mifupa ya mfalme wa Edomu hata ikawa chokaa;
2. lakini nitapeleka moto juu ya Moabu, nao utayateketeza majumba ya Keriothi; na Moabu atakufa pamoja na mshindo, na kelele, na sauti ya tarumbeta;
3. nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema Bwana.
4. Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata;
5. lakini nitapeleka moto juu ya Yuda, nao utayateketeza majumba ya Yerusalemu.
6. Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;
7. nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya mwenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu;
8. nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha.
9. Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini.
10. Pia naliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arobaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori.
11. Nami nikawainua watu miongoni mwa wana wenu wawe manabii, na katika vijana wenu wawe Wanadhiri; je! Sivyo hivyo, enyi wana wa Israeli? Asema Bwana.
12. Lakini mliwapa Wanadhiri mvinyo wanywe; mkawaamuru manabii, mkisema, Msifanye unabii.
13. Tazameni, nitawalemea ninyi, Kama gari lilemeavyo lililojaa miganda.
14. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake;
15. Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake;
16. Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa Atakimbia uchi siku ile, asema Bwana.

  Amos (2/9)