← Acts (9/28) → |
1. | Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, |
2. | akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. |
3. | Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. |
4. | Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? |
5. | Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. |
6. | Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. |
7. | Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. |
8. | Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. |
9. | Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. |
10. | Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. |
11. | Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; |
12. | naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. |
13. | Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; |
14. | hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. |
15. | Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. |
16. | Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. |
17. | Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. |
18. | Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa; |
19. | akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski. |
20. | Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. |
21. | Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? |
22. | Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. |
23. | Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; |
24. | lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. |
25. | Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu. |
26. | Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. |
27. | Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. |
28. | Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. |
29. | Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua. |
30. | Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso. |
31. | Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. |
32. | Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida. |
33. | Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. |
34. | Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka. |
35. | Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana. |
36. | Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. |
37. | Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. |
38. | Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. |
39. | Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. |
40. | Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. |
41. | Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. |
42. | Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana. |
43. | Basi Petro akakaa siku kadha wa kadha huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi. |
← Acts (9/28) → |