← Acts (7/28) → |
1. | Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? |
2. | Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, |
3. | akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha. |
4. | Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa. |
5. | Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto. |
6. | Mungu akanena hivi, ya kwamba wazao wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne. |
7. | Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. |
8. | Akampa agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu. |
9. | Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, |
10. | akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote. |
11. | Basi kukawa njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. |
12. | Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. |
13. | Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao. |
14. | Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano. |
15. | Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu; |
16. | wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kima cha fedha kwa wana wa Hamori, huko Shekemu. |
17. | Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri, |
18. | hata mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu. |
19. | Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi. |
20. | Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye. |
21. | Hata alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe. |
22. | Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo. |
23. | Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli. |
24. | Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri. |
25. | Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. |
26. | Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? |
27. | Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? |
28. | Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana? |
29. | Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko. |
30. | Hata miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika mwali wa moto, kijitini. |
31. | Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia, |
32. | Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama. |
33. | Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. |
34. | Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri. |
35. | Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. |
36. | Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini. |
37. | Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye. |
38. | Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi. |
39. | Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarejea Misri, |
40. | wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui lililompata. |
41. | Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono yao. |
42. | Basi Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika chuo cha manabii, Je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadaka Miaka arobaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli? |
43. | Nanyi mlichukua hema ya Moleki, Na nyota za mungu wenu Refani, Sanamu mlizozifanya ili kuziabudu; Nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli. |
44. | Ile hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawasawa na mfano ule aliouona; |
45. | ambayo baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi; |
46. | aliyepata fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. |
47. | Lakini Sulemani alimjengea nyumba. |
48. | Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii, |
49. | Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana, |
50. | Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote? |
51. | Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. |
52. | Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua; |
53. | ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike. |
54. | Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. |
55. | Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. |
56. | Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. |
57. | Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, |
58. | wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. |
59. | Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. |
60. | Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake. |
← Acts (7/28) → |