← Acts (5/28) → |
1. | Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, |
2. | akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. |
3. | Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? |
4. | Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. |
5. | Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. |
6. | Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. |
7. | Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. |
8. | Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. |
9. | Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. |
10. | Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. |
11. | Hofu nyingi ikawapata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya. |
12. | Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; |
13. | na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; |
14. | walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; |
15. | hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. |
16. | Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa. |
17. | Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, |
18. | wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; |
19. | lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, |
20. | Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. |
21. | Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. |
22. | Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, |
23. | wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. |
24. | Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. |
25. | Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. |
26. | Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe. |
27. | Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, |
28. | akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. |
29. | Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. |
30. | Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. |
31. | Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. |
32. | Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. |
33. | Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua. |
34. | Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, |
35. | akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. |
36. | Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. |
37. | Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. |
38. | Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, |
39. | lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. |
40. | Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. |
41. | Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. |
42. | Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo. |
← Acts (5/28) → |