← Acts (26/28) → |
1. | Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea, |
2. | Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi. |
3. | Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu. |
4. | Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu, |
5. | wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa. |
6. | Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi baba zetu waliyopewa na Mungu, |
7. | ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme. |
8. | Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu? |
9. | Kweli, mimi mwenyewe naliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingamana na jina lake Yesu Mnazareti; |
10. | nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nalitoa idhini yangu. |
11. | Na mara nyingi katika masinagogi yote naliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini. |
12. | Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; |
13. | Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. |
14. | Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. |
15. | Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. |
16. | Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; |
17. | nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; |
18. | uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi. |
19. | Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni, |
20. | bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao. |
21. | Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata ndani ya hekalu wakajaribu kuniua. |
22. | Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa; |
23. | ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa. |
24. | Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. |
25. | Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili. |
26. | Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni. |
27. | Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. |
28. | Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. |
29. | Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi. |
30. | Mfalme na liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama; |
31. | hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa. |
32. | Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari. |
← Acts (26/28) → |