← Acts (24/28) → |
1. | Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza liwali habari za Paulo. |
2. | Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa maangalizi yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya taifa hili, |
3. | basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote. |
4. | Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako. |
5. | Kwa maana tumemwona mtu huyu mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazorayo. |
6. | Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu. |
7. | Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu, |
8. | Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwuliza-uliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi. |
9. | Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo. |
10. | Na liwali alipompungia mkono ili anene, Paulo akajibu, Kwa kuwa ninajua ya kwamba wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea mwenyewe kwa moyo wa furaha. |
11. | Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu ili kuabudu. |
12. | Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihojiana na mtu, au kufanya fujo katika mkutano, wala katika masinagogi wala ndani ya mji. |
13. | Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa. |
14. | Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii. |
15. | Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia. |
16. | Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote. |
17. | Baada ya miaka mingi nalifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo. |
18. | Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, hali nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia, |
19. | ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lo lote juu yangu. |
20. | Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza, |
21. | isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo. |
22. | Basi Feliki aliwaahirisha, kwa sababu alijua habari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lisia jemadari atakapotelemka nitakata maneno yenu. |
23. | Akamwamuru yule akida kwamba Paulo alindwe; ila awe na nafasi, wala asimkataze mmojawapo wa rafiki zake kumtumikia. |
24. | Baada ya siku kadha wa kadha, Feliki akafika pamoja na Drusila mkewe aliyekuwa Myahudi, akatuma kumwita Paulo akamsikiliza habari za imani iliyo kwa Kristo Yesu. |
25. | Na Paulo alipokuwa akitoa hoja zake katika habari ya haki, na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akafanya hofu akajibu, Sasa enenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita. |
26. | Pamoja na hayo alitaraji kwamba atapewa fedha na Paulo; kwa hiyo alimwita mara nyingi akaongea naye. |
27. | Na miaka miwili ilipotimia, Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paulo amefungwa. |
← Acts (24/28) → |