← Acts (2/28) → |
1. | Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. |
2. | Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. |
3. | Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. |
4. | Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. |
5. | Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. |
6. | Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. |
7. | Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? |
8. | Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? |
9. | Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, |
10. | Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, |
11. | Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. |
12. | Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? |
13. | Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya. |
14. | Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. |
15. | Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; |
16. | lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, |
17. | Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. |
18. | Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. |
19. | Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. |
20. | Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri. |
21. | Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. |
22. | Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; |
23. | mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; |
24. | ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. |
25. | Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. |
26. | Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. |
27. | Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. |
28. | Umenijuvisha njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako. |
29. | Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. |
30. | Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi; |
31. | yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. |
32. | Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake. |
33. | Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia. |
34. | Maana Daudi hakupanda mbinguni; bali yeye mwenyewe anasema, |
35. | Hata nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako. |
36. | Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo. |
37. | Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? |
38. | Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. |
39. | Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. |
40. | Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. |
41. | Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. |
42. | Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. |
43. | Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume. |
44. | Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, |
45. | wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. |
46. | Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, |
47. | wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa. |
← Acts (2/28) → |