| ← Acts (16/28) → |
| 1. | Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. |
| 2. | Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. |
| 3. | Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani. |
| 4. | Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. |
| 5. | Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. |
| 6. | Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. |
| 7. | Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, |
| 8. | wakapita Misia wakatelemkia Troa. |
| 9. | Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. |
| 10. | Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema. |
| 11. | Basi tukang'oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; |
| 12. | na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. |
| 13. | Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. |
| 14. | Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. |
| 15. | Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha. |
| 16. | Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. |
| 17. | Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. |
| 18. | Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile. |
| 19. | Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji; |
| 20. | wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; |
| 21. | tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi. |
| 22. | Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. |
| 23. | Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. |
| 24. | Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. |
| 25. | Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. |
| 26. | Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. |
| 27. | Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. |
| 28. | Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. |
| 29. | Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; |
| 30. | kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? |
| 31. | Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. |
| 32. | Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. |
| 33. | Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo. |
| 34. | Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu. |
| 35. | Kulipopambauka makadhi wakawatuma wakubwa wa askari wakisema, Waacheni watu wale waende zao. |
| 36. | Yule mlinzi wa gereza akamwarifu Paulo maneno haya akisema, Makadhi wametuma watu ili mfunguliwe; basi, sasa tokeni nje, enendeni zenu kwa amani. |
| 37. | Paulo akawaambia, Wametupiga mbele ya watu wote bila kutuhukumu, na sisi tu Warumi, tena wametutupa gerezani; na sasa wanataka kututoa kwa siri? Sivyo, lakini na waje wenyewe wakatutoe. |
| 38. | Wakubwa wa askari wakawapasha makadhi habari za maneno haya; nao wakaogopa, waliposikia ya kwamba hao ni Warumi. |
| 39. | Wakaja wakawasihi; na walipokwisha kuwatoa nje, wakawaomba watoke katika mji ule. |
| 40. | Nao wakatoka gerezani wakaingia nyumbani mwa Lidia; na walipokwisha kuonana na ndugu wakawafariji, wakaenda zao. |
| ← Acts (16/28) → |