| ← Acts (11/28) → |
| 1. | Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. |
| 2. | Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, |
| 3. | wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. |
| 4. | Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, |
| 5. | Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia. |
| 6. | Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. |
| 7. | Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. |
| 8. | Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. |
| 9. | Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. |
| 10. | Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. |
| 11. | Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. |
| 12. | Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; |
| 13. | akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, |
| 14. | atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. |
| 15. | Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. |
| 16. | Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu. |
| 17. | Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? |
| 18. | Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima. |
| 19. | Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. |
| 20. | Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. |
| 21. | Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. |
| 22. | Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. |
| 23. | Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. |
| 24. | Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. |
| 25. | Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; |
| 26. | hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. |
| 27. | Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. |
| 28. | Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. |
| 29. | Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi. |
| 30. | Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli. |
| ← Acts (11/28) → |