Acts (1/28) → |
1. | Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, |
2. | hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; |
3. | wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. |
4. | Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; |
5. | ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. |
6. | Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? |
7. | Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. |
8. | Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. |
9. | Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. |
10. | Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, |
11. | wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni. |
12. | Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. |
13. | Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. |
14. | Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake. |
15. | Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, |
16. | Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu; |
17. | kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. |
18. | (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka. |
19. | Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.) |
20. | Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; |
21. | Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, |
22. | kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. |
23. | Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. |
24. | Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, |
25. | ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. |
26. | Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja. |
Acts (1/28) → |