| ← 2Thessalonians (3/3) |
| 1. | Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; |
| 2. | tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. |
| 3. | Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. |
| 4. | Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya. |
| 5. | Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo. |
| 6. | Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu. |
| 7. | Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; |
| 8. | wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. |
| 9. | Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. |
| 10. | Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. |
| 11. | Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. |
| 12. | Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. |
| 13. | Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema. |
| 14. | Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari; |
| 15. | lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu. |
| 16. | Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote. |
| 17. | Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila waraka, ndio mwandiko wangu. |
| 18. | Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote. |
| ← 2Thessalonians (3/3) |