2Thessalonians (1/3)  

1. Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo.
2. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo.
3. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi.
4. Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili.
5. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa.
6. Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi;
7. na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake
8. katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;
9. watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;
10. yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu).
11. Kwa hiyo twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu;
12. jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

      2Thessalonians (1/3)