← 2Samuel (13/24) → |
1. | Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. |
2. | Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote. |
3. | Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. |
4. | Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, umbu la ndugu yangu, Absalomu. |
5. | Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake. |
6. | Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. |
7. | Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula. |
8. | Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate. |
9. | Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake. |
10. | Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. |
11. | Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. |
12. | Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. |
13. | Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. |
14. | Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. |
15. | Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. |
16. | Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. |
17. | Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. |
18. | Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. |
19. | Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti. |
20. | Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu. |
21. | Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana. |
22. | Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari. |
23. | Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme. |
24. | Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumwa wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumwa wako. |
25. | Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki. |
26. | Ndipo akasema Absalomu, Kwamba huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi. |
27. | Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye. |
28. | Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri. |
29. | Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia. |
30. | Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. |
31. | Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa. |
32. | Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari. |
33. | Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. |
34. | Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake. |
35. | Ndipo Yonadabu akamwambia mfalme, Tazama, wana wa mfalme wamekuja; kama mimi mtumwa wako nilivyosema, ndivyo ilivyo. |
36. | Ikawa alipokwisha kusema, tazama, wana wa mfalme walikuja, nao wakapaza sauti zao wakalia; mfalme naye akalia, na watumishi wake wote, kilio kikubwa mno. |
37. | Lakini Absalomu akakimbia, akamwendea Talmai, mwana wa Amihuri, mfalme wa Geshuri. Naye Daudi akamlilia mwanawe kila siku. |
38. | Basi Absalomu akakimbia, akaenda Geshuri, akakaa huko muda wa miaka mitatu. |
39. | Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa. |
← 2Samuel (13/24) → |