2Samuel (1/24)  

1. Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi;
2. hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia.
3. Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli.
4. Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.
5. Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?
6. Yule kijana aliyempa habari akasema, Nalikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama, Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi wanamfuatia kwa kasi.
7. Naye alipotazama nyuma, akaniona, akaniita. Nikajibu, Mimi hapa.
8. Akaniambia, U nani wewe? Nikamjibu, Mimi ni Mwamaleki.
9. Akaniambia, Tafadhali simama karibu nami, ukaniue, maana shida imenipata; kwa sababu roho yangu ingali hai ndani yangu.
10. Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.
11. Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye;
12. wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga.
13. Naye Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Watoka wapi wewe? Akajibu, Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.
14. Daudi akamwambia, Jinsi gani hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi
15. Ndipo Daudi akamwita mmoja wa vijana, akamwambia, Mwendee, ukamwangukie. Basi akampiga hata akafa.
16. Daudi akamwambia, Damu yako na iwe juu ya kichwa chako mwenyewe; maana umejishuhudia nafsi yako ukisema, Nimemwua masihi
17. Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya;
18. (kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yashari), akasema, Wana wa Yuda na wafundishwe haya,
19. Walio fahari yako, Ee Israeli Juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; Jinsi mashujaa walivyoanguka!
20. Msiyahubiri mambo haya katika Gathi, Msiyatangaze katika njia za Ashkeloni; Wasije wakashangilia binti za Wafilisti, Binti za wasiotahiriwa wakasimanga.
21. Enyi milima ya Gilboa, visiwepo juu yenu Umande wala mvua, wala mashamba ya matoleo; Maana ndipo ilipotupwa kwa aibu ngao ya shujaa, Ngao yake Sauli, pasipo kutiwa mafuta.
22. Kutoka kwa damu yao waliouawa, Kutoka kwa shahamu yao mashujaa, Upinde wa Yonathani haukurudi nyuma, Wala upanga wa Sauli haukurudi bure.
23. Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza Maishani wala mautini hawakutengwa; Walikuwa wepesi kuliko tai, Walikuwa hodari kuliko simba.
24. Enyi binti za Israeli, mlilieni Huyo Sauli, ambaye aliwavika Mavazi mekundu kwa anasa, Akazipamba nguo zenu dhahabu.
25. Jinsi mashujaa walivyoanguka Katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa Juu ya mahali pako palipoinuka
26. Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake.
27. Jinsi mashujaa walivyoanguka, Na silaha za vita zilivyoangamia!

      2Samuel (1/24)