2John (1/1)    

1. Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;
2. kwa ajili ya hiyo kweli ikaayo ndani yetu, nayo itakuwa pamoja nasi hata milele.
3. Neema, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.
4. Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba.
5. Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane.
6. Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo.
7. Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.
8. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu.
9. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.
10. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.
11. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.
12. Kwa kuwa ninayo mambo mengi, sitaki kuyaandika kwa karatasi na wino; lakini nataraji kuja kwenu, na kusema nanyi uso kwa uso, ili furaha yetu iwe imetimizwa.
13. Watoto wa ndugu yako aliye mteule, wakusalimu.

      2John (1/1)